Familia ya Sharo yaibua mazito
Hussein Ramadhani Mkiety (Sharo Milionea) |
FAMILIA ya msanii Hussein Ramadhani Mkiety (Sharo Milionea)
aliyekufa katika ajali wilayani Muheza wiki
iliyopita imedai kuwa
haiamini kwamba kifo cha mtoto huyo kilitokana na ajali, hivyo kulitaka
Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kubaini ukweli.
Mjomba wa marehemu , Mohamed Msenga alisema jana kwamba familia imekuwa na shaka juu ya mazingira ya kifo hicho baada ya kurejeshewa nguo za msanii huyo zilizokuwa zimeibwa baada ya ajali lakini hazikuwa na damu.
Msenga alisema muda mfupi baada ya mama mzazi wa Marehemu Zaina Mwaimu Mkiety (54), kuitwa polisi na kukabidhiwa vitu mbalimbali zikiwamo nguo ambazo marehemu alikuwa amevaa siku ya ajali hawakuona hata alama ya damu jambo ambalo liliwashangaza.
Alisema shaka hiyo ilianzia katika eneo ambalo ajali hiyo ilitokea akisema walipofika na kuonyeshwa mahala alipokuwa ameangukia, hawakuona damu jambo ambalo liliwatia shaka.
Alisema begi la nguo za msanii huyo lilikuwa na udongo mwingi likionyesha kwamba walioiba walikuwa wamelifukia kabla ya kusalimisha lakini hakuna damu zilizoonekana.
Soma zaidi ........
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Teule Muheza, Dk Julius Mjema aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Sharo Milionea alisema sababu ya kifo chake ni kichwa kupondeka.
“Mimi ndiye niliyefanyia ‘postmoterm’ (uchunguzi), mwili wa Sharo Milionea, ni kwamba kichwa kilikuwa kimepondeka huku mifupa ya kichwa ikiwa imepondeka pia,” alisema Dk Mjema.
Kuhusu madai ya nguo kutokuwa na damu, alisema marehemu alipata mpasuko wa ndani kwa ndani na siyo wa nje, ndiyo maana alipofikishwa chumba cha maiti damu zilionekana zikiwa zimeganda masikioni.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alipoulizwa kuhusu madai hayo ya familia alisema: “Hiyo ni taarifa ambayo jeshi la polisi litaifanyia kazi kwa kuingia kwa kina katika kuchunguza ili kuridhisha pande zote.”
Mama yake alia kukosa mjukuu
Katika hatua nyingine, mama mzazi wa msanii huyo amesema kutoachiwa mjukuu na tarehe za mwisho wa mwezi ni alama ambazo zitasababisha awe akimkumbuka mwanaye huyo milele. Akizungumza nyumbani kwake, katika Kitongoji cha Jibandeni Kijiji cha Lusanga wilayani hapa alisema kila ulipokuwa ukifikia mwisho wa mwezi ulikuwa ni muda wake wa neema kwani Sharo Milionea alimtumia fedha za matumizi yake binafsi pamoja na familia nzima nyumbani hapo.
“Pamoja na kwamba kila mara alikuwa akinitumia
fedha za kutatua shida zangu mbalimbali nilizokuwa nikimweleza lakini
kila mwisho wa mwezi alikuwa akihakikisha anatuma fungu la matumizi
yangu na ndugu zake hapa nyumbani,” alisema mama huyo.
Alisema mwisho wa
mwezi itakuwa ni alama ya kudumu ya kumbukumbu ya mwanawe kwa sababu ni
wakati ambao alikuwa akimtumia fedha za matumizi yake pamoja na
familia
nzima.
Kuhusu mjukuu alisema: “Sharo ni mwanangu wa pekee wa kiume, amekufa bila kuniachia mjukuu.. hii inaniuma sana lakini namshukuru Mungu kwani amechukua kiumbe chake na ndiye ajuaye siri iliyofichika mbele yangu,” alisema.
Alisema hadi alipofariki hakuwahi kumdokeza juu ya kuwa na mtoto wala kumpa mimba msichana yeyote... “Unajua Sharo Milionea alizaliwa pacha na mwenzake Hassan lakini mwenzake alifariki dunia siku tano baada ya kuzaliwa kwa hiyo katika kizazi changu mwanangu pekee wa kiume alikuwa Sharo Milionea ambaye nilitumaini kwamba angeniletea wajukuu,” alisema Zaina.
Alisema Sharo Milionea amekufa kabla hajatekeleza ndoto yake ya kumjengea nyumba ya kisasa pamoja na kuweka miradi ya kuboresha maisha yake azma ambayo aliiweka mwezi mmoja kabla ya kupata ajali iliyotoa uhai wake.
Atoa ya moyoni kwa walioshiriki msiba
Zaina alitoa shukrani za pekee kwa Rais Jakaya Kikwete na mkewe, Salma kwa kutuma ujumbe maalumu pamoja na rambirambi kutokana na msiba wa mwanaye huyo. Pia alimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, wasanii, waandishi wa habari na kampuni mbalimbali zilizoshiriki pamoja na kutuma salamu za rambirambi.
“Kwa kweli katika maisha yangu sikuwahi kudhani wala kuhisi kama
Hussein angeweza kuwa maarufu kiasi hiki cha kusababisha hadi Rais wa
nchi na mkewe kutuma ujumbe maalumu wa kuja hapa kijijini, ni jambo
lililonishangaza sana,” alisema Zaina.
Alisema alifarijika na kuwapo kwa King Majuto na kundi lake hasa kutokana na hatua yao ya kuuchukulia msiba huo kama wa kwao kwa kuendelea kubaki kijijini hapo baada ya mazishi hadi iliposomwa tatu. Alisema kifo cha mwanaye kimempa funzo kwamba sanaa ni zaidi ya baadhi ya watu wanavyoichukulia akisema inamwezesha anayejituma kupata umaarufu wa haraka.
Alisema alifarijika na kuwapo kwa King Majuto na kundi lake hasa kutokana na hatua yao ya kuuchukulia msiba huo kama wa kwao kwa kuendelea kubaki kijijini hapo baada ya mazishi hadi iliposomwa tatu. Alisema kifo cha mwanaye kimempa funzo kwamba sanaa ni zaidi ya baadhi ya watu wanavyoichukulia akisema inamwezesha anayejituma kupata umaarufu wa haraka.
Alisifu umoja na mshikamano ulioonyeshwa na wasanii katika msiba huo. Afafanua wasifu
Mama huyo alisema amekuwa akishangazwa na baadhi ya watu kupotosha juu ya wasifu wa mwanaye huyo. Alisema Hussein alizaliwa mwaka 1987 hapohapo Jibandeni na baadaye alijiunga na Shule ya Msingi Lusanga ambako alihitimu darasa la saba mwaka 2003.
Baada ya kuhitimu darasa la saba, Hussein alikwenda Dar es Salaam kumfuata mama yake huyo aliyekuwa akiishi Kiwalani. “Kwa kipindi kirefu alikuwa anahangaika bila ya kuwa na cha kufanya. Baadaye mjomba wake aliamua kumnunulia vifaa vya ufundi wa magari akamlipia ada ili ajiunge na gereji aliyomtafutia kwa ajili ya mafunzo,” alisema Zaina. Alisema hata hivyo, baada ya kukabidhiwa zana hizo, Hussein alimweleza mama yake kwamba hadhani kama angeweza kufanya kazi hiyo akisema hakuwa na moyo huo. “Alikwenda kama siku mbili tu gereji, siku iliyofuata nilimwamsha asubuhi awahi, lakini akaniambia mimi sielewi na maspana yao nimewaachia siendi tena,” alisema Zaina.
Alisema baada ya hapo akaanza kuchukua
redio nyumbani na kwenda nayo kujifunza mambo ya sanaa.
Mwaka 2006 mama
huyo alisema aliamua kurejea kijijini Lusanga kutokana na maisha kumwia
magumu, lakini alisema Sharo Milionea aliamua kubaki hapohapo Kiwalani
ambako majirani walimhakikishia kuwa watamtunza.
“Nikiwa Kijijini
Lusanga nilishangaa siku moja akinipigia simu na kusema anataka
kunitumia simu, baada ya hapo ikawa ndiyo mwanzo wa neema kwani
alinitumia fedha mara kwa mara,” alisema Zaina.
Sharo alilea kijana
yatima
Marehemu Sharo Milionea alikuwa akiishi na kijana yatima aliyekuwa akimlea kwa kumlipia ada na kumhudumia kwa mambo yote ya kimaisha. Kijana huyo, Said Kassim ambaye amemaliza kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Turiani iliyopo Magomeni, Dar es Salaam alisema alimjua Sharo Milionea baada ya kutokea kifo cha mama yake mzazi aliyekuwa akiishi naye na wanafunzi wenzake walipoona akihangaika kutokana na maisha magumu walimpeleka kwa msanii huyo na kumwomba amsaidie.
“Waliponipeleka kwa kaka Sharo, alinipokea
na kusema kuanzia siku ile nikae naye nyumbani kwake, akawa ananihudumia
kwa kila kitu. Alinilipia
ada shuleni, kuninunulia nguo sasa amekufa
sijui nitafanyaje,” alisema na kuanza kutokwa machozi.
Said alisema hadi
mama yake alipofariki dunia, hakuwahi kumtajia baba yake hivyo alimwona
Sharo Milionea kama ndiye mkombozi wake wa maisha.
Alisema kabla ya
kifo chake, Sharo Milionea aliahidi
kumfungulia duka la nguo na
kumpeleka kwenye chuo cha kompyuta ili aweze kuwa na ujuzi wa kuendesha
miradi ya msanii huyo.
Familia ya Sharo yaibua mazito
Reviewed by Unknown
on
Thursday, December 06, 2012
Rating:
No comments: